Kuelekea Msimu mpya wa Kilimo Wilaya ya Hanang TPHPA na FAO wajitosa kunusuru matumizi makubwa ya rasilimali wakati wa uzalishaji
Na Innocent Natai
Kuelekea msimu mpya Mpya wa Kilimo Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na kilimo la umoja wa mataifa (FAO) wametoa elimu ya namna ya kudhibiti Visumbufu vya Mimea aina ya Viwavijeshi Kwa wakulima Mfano Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara ili kuwasaidia kuepukana na athari za matumizi makubwa ya rasilimali fedha na muda wakati wa kupambana na visumbufu hivyo.
Akizungumza baada ya Mafunzo hayo Bi Gress Matiku ambaye ni mtaalamu wa kudhibiti visumbufu vya Mlipuko kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) amesema kuwa mafunzo hayo yamejumuisha wakulima Ishirini na Tano (25) na Maafisa Ugani kutoka Kata mbalimbali za Wilaya hiyo na dhumuni la mafunzo hayo ikiwa ni kutoa elimu ya udhibiti Shirikishi ya kudhibiti Viwavijeshi Vamizi.
Amesema kuwa mafunzo hayo yamejumuisha elimu ya kuchagua mbegu bora,kumtambua viwavijeshi, hatua sahihi ya kumdhibiti, Kutambua viuatilifu sahihi vya kumdhibiti na matumizi yaliyo sahihi ya Viuatilifu ikiwa ndio njia ya mwisho ya kumdhibiti viwavijeshi ikiwa visumbufu vitakuwa hatari zaidi
“Tulianza na wakulima kumi ambao tulichagua na tukawapa mafunzo ya kudhibiti hawa viwavijeshi tukawafundisha njia Tano za Udhibiti wa hawa Viwavijeshi kwa Vitendo na leo tuponao hapa tumewatumia kuwafundisha wengine” Alisema Bi Matiku
Aidha aliongeza kuwa Wakulima hao wamepatiwa mafunzo ya njia hizo za udhibiti ikiwemo udhibiti sango (kuandaa shamba mapema, kuchagua mbegu bora, kupanda wakati wa mvua za kwanza na kuweka mbolea ) Udhibiti kinzani kwa kutumia mbegu zinazokinzana na Viwavijeshi, kutumia njia za kibaiolojia kwa maana ya kutumi wadudu marafiki wanaowala viwavijeshi, kutumia sukuma vuta (kupanda majani yanayowafukuza nondo/Vipepeo wa viwavijeshi wasitage katika shamba) kutumia Viuatilifu vya Kibaiolojia na Mwisho kutumia Viuatilifu vya Kemikali kwa Usahihi na iwe njia ya Mwisho
Bwana Mpona Malonzo Ambaye ni Afisa Kutoka Shirika la Chakula na kilimo la umoja wa mataifa (FAO) amesema kuwa Mwitikio wa kupokea Mafunzo hayo umekuwa mkubwa Kwa wakulima kwani visumbufu hivyo vilikuwa vikiwa adhiri katika kilimo na wasijue namna ya kuvidhibiti kwa njia nafuu na sasa wamepata elimu ya namna ya kutumia pembejeo chache na kupata ufanisi katika kilimo tofauti na hapo awali
Amesema kuwa Shirika hilo limekuwa likiweka jitihada kubwa za kuwasaidia wakulima hapa nchini kwa kuwezesha tafiti mbalimbali za kudhibiti kisumbufu hicho na tayari wamesha saidia kutambuliwa kwa Wadudu marafiki wanaoweza kupambana na kisumbufu hicho bila hata kutumia kemikali na tayari wamesha sambaza wadudu hao kwa Wakulima
Ameongeza kuwa Kwa kushirikiana na Chuo cha Sokoine na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania( TPHPA) wameshaanza kuwazalisha na wamekuwa na ufanisi mkubwa huku matarajio yao ikiwa ni kuona serikali inawazalisha zaidi na kuwasambaza kwa wakulima nchini
Kwa upande wao wakulima wameshukuru Shirika hilo na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania( TPHPA) kwani walikuwa wakitumia muda mwingi,rasilimali nyingi ikiwemo fedha na muda na hata kupoteza ubora wa mazao yako kwa kukosa elimu ya udhibiti wa viwavijeshi
Kwa mara ya kwanza Viwavijeshi Vamizi walionekana Tanzania mwaka 2017 katika Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa na Mpaka sasa viwavijeshi vamizi wamefika zaidi ya mikoa 15 ya Tanzania, Takwimu zilizotolewa na Kituo cha Kimataifa cha Kilimo na Bioscience (CABI) mwaka 2017 zinasema tangu Viwavijeshi avamie barani Afrika Mwaka 2016 amesababisha hasara ya kiasi cha takribani $13.383 M kwa mazao kama mahindi, mtama na miwa ikiwa ni nje ya mimea aina 80 inayoshambuliwa na mdudu huyo
Comments
Post a Comment