TPHPA yazidi kusonga mbele Zoezi la Udhibiti wa Panya waharibifu Mkoa wa Morogoro //Wakulima wapongeza
Na Innocent Natai
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Afya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imefanikiwa kuokoa zaidi ya Ekari 931,920 Mkoani Morogoro zilizovamiwa na Panya waharibifu na kuziwezesha Kaya 1682 kuwa na uhakika wa kupata mavuno na usalama wa mavuno yao baada ya kuyatoa shambani.
Akizungumza wakati wakiendelea na zoezi hilo lililoanza Septemba 23,2023 Kaimu Mkuu wa Kituo cha kudhibiti Baa la Panya TPHPA (Morogoro) Bi. Christina Tewele amesema zoezi hilo linaendelea vizuri na wapo ukingoni kulitamatisha kwa kuhakikisha wanadhibiti mlipuko huo wa Panya waharibifu ili kuwasaidia wakulima kuepukana na upotevu wa mazao yao kabala na baada ya mavuno
Amesema Mamlaka hiyo imefanya kazi ya udhibiti wa panya hao kwa awamu Mbili (2) mwezi Agosti na Septemba na Jumla ya kata zoezi hilo lilipofanyika ni Nane (8)
na Jumla ya vijiji Ishirini na Mbili (22) vyenye jumla ya kaya zilizochanga chambo 1682 vimehudumiwa.
"chambo kilichochangwa ni 15,532kg mpaka sasa kwa chambo hicho tumefanikiwa kudhibiti ekari 931,920 na matokeo ni mazuri, tumefanikiwa kuwadhibiti kikamilifu"amesema Bi Christina Tewele
Amesema mikakati yao TPHPA ni kuhakikisha Mkulima anafurahia kushiriki katika kilimo, hivyo watatoa ushirikiano pale watakapohitajika.
Aidha amezitaka Halmashauri zinazopatwa na Milipuko ya visumbufu hivyo kutoa taarifa mapema kwa Mamlaka hiyo ili iweze kuwahi kutoa huduma kabla havijaleta madhara makubwa kwa wakulima kwani zoezi la udhibiti ni mchakato na linahitaji taarifa za haraka
Kwa upande wake aliyekuwa mratibu wa zoezi hilo Ndugu Maulid Chatto amesema kuwa zoezi hilo limeenda vizuri na wamefanikiwa kudhibiti katika yale maeneo yaliyokuwa na uvamizi mkubwa na sasa wamebakisha maeneo yenye uvamizi mdogo huku wakiendelea kupokea taarifa za maeneo mengine kama yatapata uvamizi
Aidha ameongeza kuwa Mamlaka hiyo imekuwa ikiweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha wakulima wanapata huduma ya udhibiti kwa haraka ikiwemo kuwataka wakulima hao kuandaa chambo (pumba, dagaa na mafuta) ambapo baada ya kuandaa wao huja kupima uzani, kuwapa elimu ya matumizi, kuwachanganyia kiuatilifu na baada ya hapo kuwapa ili wakaweke kwenye mashamba yao.
Wakulima na viongozi wa Maeneo yaliyofanyiwa udhibiti Mkoani hapo wameishukuru Mamlaka hiyo na Serikali kwa ujumla kwa kuwasaidia kudhibiti kwani kutokana na wingi wa panya hao walishaanza kuleta madhara kwenye mazao hayo
Comments
Post a Comment