TPHPA KUFIKIA MALENGO YA KUBORESHA AFYA ZA WALAJI











Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania  TPHPA imefanikiwa kuweka mikakati ya msingi inayolenga kuzalishwa mazao yasiyo na masalia ya Viuatilifu

ili kupanua wigo katika soko la dunia kwa mustakabali wa kulinda afya za Binadamu na Mazingira.


Akizungumza katika Mkutano wa Mwaka wa Wadau wa  Afya ya Mimea na Viuatilifu Uliofanyika Juni 21. 2024 katika Ukumbi wa Makao Makuu ya Mamlaka hiyo Ngaramtoni, Jijini Arusha ambao hufanyika kila mwaka, Mkuu wa  Wilaya ya Arumeru Emmanuela Kaganda akimwakilisha Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliyetarajiwa kuwa Mgeni Rasmi, ameipongeza Mamlaka hiyo kwa jitihada zake kubwa za kuleta mabadiliko na uzalishaji wenye tija  katika Sekta ya Kilimo.


Aidha ameongeza kuwa, Sekta ya Kilimo ni mkombozi kwani inategemewa kuongeza ajira za vijana na wanawake, kutoa ajira za stara, kuimarisha mfumo wa chakula na kuongeza pato la taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.


"Serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta hii muhimu imeongeza bajeti kutoka bilioni 970 kwa mwaka wa fedha  2023-2024 kufikia tilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2024-2025, hii yote ni kuhakikisha tunajiimarisha katika soko la dunia na kuzidi kuwa bora katika uzalishaji wa chakula cha kutosha" amesema,


"Nawasisitiza Mamlaka ya TPHPA kuhifadhi mbegu za asili, hii itasaidia kuepuka upotevu wa mbegu bora zinazotegemewa katika ushindani wa soko la dunia" amesisitiza Kaganda.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPHPA Prof. Andrew Temu amesema kuna muelekeo wa mamlaka hiyo kutimiza malengo yake ya kuboresha afya za watu kutokana na juhudi na mikakati mbambali inayowekwa.


Ameongeza kwamba, TPHPA inatambua juhudi za serikali katika utekelezaji wa majukumu yao, ushauri na maelekezo muhimu yenye lengo la kuhakikisha mamlaka hiyo inaimarika na kuendelea kufanya vizuri.


"Tunaendelea na jitihada za kutanua wigo wa kilimo cha umwagiliaji lakini pia kupambana na changamoto mbalimbali zikiwemo usugu wa viuatilifu, kupotea kwa vinasaba katika mimea ya asili, ubunifu na mbinu   juu ya viuatilifu sambamba na hayo tunajipanga kwa matumizi ya akili mnemba ili kuendana na Maendeleo ya Teknolojia lakini pia kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi" ameeleza Prof. Temu.


Vivyo hivyo Mkurugenzi wa TPHPA Prof. Joseph Ndunguru ameeleza kuwa, mkutano huu umetoa fursa kwa wadau wa sekta ya kilimo kubadilishana uzoefu, changamoto na ushauri katika kuleta mageuzi kwa sekta hiyo.


"Naishukuru kamati ya kudumu ya Bunge, inayosimamia wizara ya Kilimo, viwanda na Biashara kwa kupitisha bajeti ambayo imetupa tumaini la kufikia malengo tuliyojiwekea TPHPA" ameeleza Prof.Ndunguru.


Pia Mmoja wa Wadau aliyeshiriki katika mkutano wa TPHPA Afisa kilimo Mohamed Hussein kutoka kampuni ya Agrimatco Tanzania LTD amesema wanashirikiana vyema na mamlaka ya TPHPA na wamekuwa wakipata elimu na  miongozo inayowasaidia kuboresha utendaji na utoaji huduma bora kwa wakulima.


"Hii mamlaka ni mkombozi wetu lakini pia inatuelekeza namna ya matumizi bora ya viuatilifu na jinsi ya kuwashauri wateja wetu ambao ni wakulima" amesema Hussein.

Mwisho.

Comments

Popular posts from this blog

Ni TPHPA tena! yatwaa tuzo Mshindi wa Kwanza

TPHPA WAKABIDHIWA MAABARA YA KISASA ILIYOGHARIMU BIL.3.8, KATIBU MKUU WIZARA YA KILIMO ATOA MAAGIZO

Kanda ya Kaskazini yatolewa kimasomaso na TPHPA Mashindano ya SHIMMUTA 2024//Yatwaa Mataji Matatu huku ikiweka rekodi Maalumu