MAFUNZO YA MATUMIZI SAHIHI NA SALAMA YA VIUATILIFU YANAYOTOLEWA NA TPHPA NI CHACHU YA AGENDA 10/30
Katibu Tawala msaidizi wa Mkoa wa Mbeya (Kitengo cha Uchumi na Uzalishaji) Ndg.Said Juma ambae alikuwa Mgeni rasmi katika hafla ya kufunga Mafunzo ya Matumizi sahihi na salama ya viuatilifu Mkoani Mbeya 30/8/2024 yanayotolewa na TPHPA amesema mafunzo haya yatasaidia sekta ya kilimo katika kutoa mchango mkubwa zaidi kwenye Agenda 10/30,hivyo mafunzo haya ni muhimu na ni chachu ya kufikia lengo hilo la agenda 10/30 na TPHPA ni wadau muhimu katika kufanikisha matokeo chanya ya kilimo nchini hususani ya agenda 10/30.
Akitahadharisha juu ya athari mbalimbali zinazotokana na ulaji wa vyakua ambavyo vimenyunyizwa viuatilifu kwa njia isiyo sahihi na salama ndg.Said amesema watu wote tunaingia kwenye kupata madhara wakiwepo wao wakulima na wafanyabiashara hivyo amewataka kila mhitimu akawe balozi mzuri wa matumizi sahihi na salama ya viuatilifu ili kuepuka madhara hayo.
Pamoja na hayo amewasihi na kuwataka washiriki wa Mafunzo wakatoe elimu ya matumizi sahihi na salama ya Viuatilifu kwa wakulima wengine na wakawashauri waende kupata mafunzo haya pindi TPHPA watakapo yatoa katika mikoa mingine.
Aidha amewataka washiriki ambao hawakufanya vizuri, wasikate tamaa bali amewaomba kama ambavyo TPHPA ilivyotoa maelezo kwamba watalelewa yaani kupewa mafunzo tena hadi pale watakapo fanya vizuri (kufikisha wastani 50%)wakubali kufanya hivyo.
Nae Mratibu wa Mafunzo haya kutoka TPHPA ndugu Rajabu Jumanne akitoa taarifa ya mafunzo katika hafla hiyo amesema jumla ya Washiriki walikuwa 111,waliofanya mtihani ni 108 na waliofahulu ni 104 ambao wanapewa vyeti ,akiongelea washiriki 4 walioshindwa amesema TPHPA itaendelea kuwalea kwa kuwajumuisha katika mafunzo mengine yanayofuata wapate tena mafunzo na kufanya mtihani ili wafikie ufahulu unaotakiwa,na watashiriki bila malipo.
Mafunzo haya ni endelevu ambapo tarehe 2/9/2024 yataendelea jijini Mwanza.
Comments
Post a Comment