Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Apongeza TPHPA kwa Mchango Mkubwa Katika Usalama wa Chakula
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mhe. Judith Nguli, ametoa pongezi kwa Uongozi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kwa juhudi zake za kipekee katika kudhibiti visumbufu vya mazao vinavyokabili wakulima wa Wilaya hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari na Maafisa wa kitengo cha habari na Mawasiliano TPHPA leo, Agosti 29, 2024 katika ofisi zake, Mhe. Nguli alisema Mamlaka hiyo imekuwa na mchango mkubwa kwa wakulima wa Wilaya hiyo kwa kupambana na visumbufu vya mazao kabla havijaleta athari kubwa kwa mazao, jambo linalopelekea usalama wa chakula na ongezeko la mazao.
“Huduma za kudhibiti visumbufu zilikuwa zinatolewa mara moja kwa mwaka, lakini tangu kuanzishwa kwa mamlaka hii, huduma hizo sasa zinatolewa mara mbili kwa misimu. Hii ni hatua muhimu katika kuongeza uzalishaji wa mazao na kuchangia katika usalama wa chakula wilayani Mvomero,” alieleza Mhe. Nguli.
Aidha, Mhe. Nguli alitoa shukrani kwa TPHPA kwa huduma nzuri zinazotolewa kwa haraka wanapohitajika katika Wilaya hiyo. Pia alitoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini, hususan kwa kuiwezesha TPHPA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Comments
Post a Comment