Naibu Waziri wa Kilimo,Mhe.David Silinde afanya ziara Kituo cha Ukaguzi cha Mamlaka Namanga//atoa Maelekezo kwa Wakaguzi
Leo, Agosti 16, 2024, Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa David Silinde, alifanya ziara ya kukagua shughuli zinazofanywa katika Kituo cha Forodha cha Pamoja (OSBP) kilichoko Namanga, mkoani Arusha. Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Silinde aliongozana na Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mheshimiwa Marko Henry Ng'umbi, na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Ndunguru, pamoja na viongozi wengine wa Mamlaka hiyo.
Katika ofisi za Ukaguzi za Mamlaka, Mheshimiwa Silinde alitoa pongezi kwa kazi zinazofanywa na wakaguzi wa Mamlaka waliopo katika ofisi hizo, akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa weledi. Alisema kuwa, shughuli hizo ni muhimu sana kwa kuhakikisha kwamba bidhaa zinazopita katika Mpaka huo zinafuata viwango vilivyowekwa, hivyo kusaidia nchi kuepuka kuingiza visumbufu na kuharibu masoko kwa kupeleka bidhaa zisizokidhi vigezo.
Mheshimiwa Silinde alihimiza wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kufanya kazi kwa bidii na umakini ili kuongeza mapato kwa nchi na kuhakikisha kwamba bidhaa zinazowasili zina ubora wa hali ya juu. Alisisitiza kwamba, kwa kufanya hivyo, nchi itakuwa na uwezo bora wa kuimarisha sekta ya kilimo na biashara kwa ujumla, hivyo kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
Comments
Post a Comment