Tanzania yaruhusiwa kuuza parachichi China







Ni furaha kwa wakulima wa parachichi chini, baada ya Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA),kufanikiwa kufungua soko la parachichi nchini China.Ruhusa hiyo imetokana na itifaki ya usafi na udhibiti wa magonjwa ya mimea iliyosainiwa mwaka 2022 kati ya Tanzania na China, ikiruhusu parachichi za Tanzania kuuzwa China.Mbali na parachichi, soko la mashudu ya alizeti pia limefunguliwa nchini China, likiwa ni sehemu ya ushirikiano wa kilimo kati ya nchi hizi mbili

Akizungumzia ruhusa hiyo leo Jumapili Septemba mosi, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru amesema hatua hiyo itaongeza wigo wa biashara ya parachichi na kuwasaidia wakulima kukuza uchumi kupitia zao hilo.
Hata hivyo, amesema licha ya ruhusa hiyo, msafirishaji wa parachichi anatakiwa awe amesajiliwe na Mamlaka ya Forodha ya China (GACC) kupitia TPHPA.

Profesa Ndunguru amesema aina za parachichi zinazoruhuswa kuingia China ni Hass, Fuerte na Pinkerton na ili kusafirisha, mashamba ya uzalishaji, ufungashaji na kampuni za kufukiza lazima pia zisajiliwe na TPHPA na wahusika watapatiwa namba ya utambulisho.

Taratibu hizo ni utekelezaji wa itifaki ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, ikihusisha usindikaji, upakiaji, uhifadhi,na usafirishaji. Profesa Ndunguru amesema mashamba yote yaliyosajiliwa lazima yafuate mbinu bora za kilimo na usimamizi wa wadudu, ili kudhibiti wadudu waharibifu kama nzi wa matunda na nondo.

Kufunguliwa kwa soko la China kunaiwezesha Tanzania kuimarisha zaidi soko la kimataifa la parachichi baada ya kufanikiwa kuteka masoko mengine barani Ulaya kama Denmark, Ufaransa, Uholanzi, Norway, Hispania, na Uingereza.

"Kuanzia sasa mashamba yote yaliyosajiliwa na yatakayosajiliwa kusafirisha parachichi kwenda China, lazima yafuate zaidi mbinu za kilimo na usimamizi jumuishi wa wadudu ili kudhibiti wadudu waharibifu kama vile nzi wa matunda na nondo," amesema.

Ikumbukwe parachichi za Tanzania pia zinauzwa Afrika Kusini na India. Tanzania sasa ni nchi ya tatu kwa uzalishaji wa parachichi barani Afrika, ikitanguliwa na Afrika Kusini na Kenya.Uzalishaji wa parachichi zinazouzwa nje ya nchi sasa umeongezeka kutoka tani 17,711.49 mwaka 2021/2022 hadi tani 26,826.3 mwaka 2022/2023.
Mauzo yake yaliongezeka kutoka dola milioni 51 za Marekani mwaka 2021/2022 hadi dola milioni 77.3 mwaka 2022/2023.

Hivi karibuni, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema ongezeko hilo limetokana na kumarika kwa soko la ndani na nje ya nchi na kwamba, Serikali kupitia taasisi zake imeimarisha utafiti wa mbegu bora za parachichi.

Comments

Popular posts from this blog

Ni TPHPA tena! yatwaa tuzo Mshindi wa Kwanza

Kanda ya Kaskazini yatolewa kimasomaso na TPHPA Mashindano ya SHIMMUTA 2024//Yatwaa Mataji Matatu huku ikiweka rekodi Maalumu

Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Apokea Makombe 6 yaliyopatikana Katika Mashindano ya Mei Mosi na SHIMMUTA 2024