TPHPA Yafanikisha kuandaa Nyaraka za Ufunguo wa Masoko Mapya kwa Mazao ya Kipaumbele Tanzania
TPHPA- Dodoma
Katika hatua muhimu kwa maendeleo ya kilimo nchini, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kwa Msaada kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) kwa kushirikiana na Muungano wa Ulaya (EU), kupitia mradi wa kuimarisha Huduma za Afya ya Mimea na Usalama wa Chakula, wamefanikiwa kuandaa nyaraka za ufikiaji wa masoko kwa mazao 8 ya kipaumbele katika nchi 14. Hafla ya uzinduzi ilifanyika tarehe 18 Septemba 2024 katika Ukumbi wa Morena Hoteli Jijini Dodoma, ikiwa na mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde.
Katika hafla hiyo, Mhe. Silinde alikabidhi nyaraka za ufunguzi wa masoko kwa Bw. Salvatory Mbilinyi, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Nyaraka hizi zinalenga kuondoa vikwazo vya usafirishaji wa mazao, ambayo kwa sasa bado hayajafikiwa kutokana na masharti ya awali yanayohitajika.
Mazao yanayohusika ni pamoja na vanilla, nanasi, parachichi, pilipili manga, kakao, na tumbaku, yanayotarajiwa kufungua fursa za kiuchumi za dola bilioni 3.5.
Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph Ndunguru, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha masoko ya kimataifa na kuzingatia viwango vya usafi. Alieleza hatua mbalimbali zinazohitajika, kama uhakiki wa viwango vya usafi na matumizi ya teknolojia mpya, ili kufanikisha malengo ya biashara.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo, na wawakilishi wa sekta binafsi, ikiwa ni ishara ya umoja katika kutekeleza mikakati ya kuimarisha sekta ya kilimo nchini Tanzania.
Comments
Post a Comment