Wakulima Waonywa Kuhusu Matumizi yasiyosahihi ya Viuatilifu






TPHPA - NJOMBE


Katika mafunzo yanayoendelea kuhusu matumizi sahihi na salama ya viuatilifu yanayofanyika Makambako, Mkoani Njombe, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imewaonya watumiaji wa viuatilifu dhidi ya tabia ya kuzidisha au kupunguza vipimo vya viuatilifu katika kunyunyuzia mazao yao.


Bwana Christian Mayige, Mkufunzi wa mafunzo haya kutoka TPHPA, alisisitiza umuhimu wa kufuata maagizo sahihi kuhusu vipimo vya viuatilifu. Katika mafunzo yake, Mayige alieleza kwamba baadhi ya wakulima wanajitahidi kuzidisha vipimo vya viuatilifu kwa dhana ya kudhibiti visumbufu kwa haraka, lakini hii inaweza kuwa hatari kwa afya ya binadamu.


"Wakulima wengi wanapenda kuzidisha vipimo vya viuatilifu wakiamini kuwa hivi ndivyo wataweza kudhibiti visumbufu kwa haraka," alisema Mayige. "Hata hivyo, hatua hii ina hatari ya kuacha viuatilifu vingi kwenye mazao, jambo ambalo si salama kwa mwanadamu."


Katika mafunzo hayo, Mayige alitoa mwongozo kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu, akisema kuwa ni muhimu kutumia viuatilifu kwa wakati na kwa kiasi kilichoelekezwa. Aliongeza kuwa kunyunyuza kwenye sehemu iliyokusudiwa ni muhimu ili kuhakikisha matokeo mazuri na salama.


Mafunzo haya yalilenga kuhakikisha kwamba watumiaji wa viuatilifu wanapata uelewa wa kina kuhusu jinsi ya kutumia viuatilifu kwa usalama na ufanisi, huku wakiepuka hatari za kiafya zinazoweza kutokea kutokana na matumizi mabaya.


Kwa kuzingatia maelekezo haya, TPHPA inaamini kwamba wakulima wataweza kudhibiti visumbufu kwa njia salama na bora, hivyo kulinda afya ya walaji na kuongeza ubora wa mazao yao.

Comments

Popular posts from this blog

Ni TPHPA tena! yatwaa tuzo Mshindi wa Kwanza

TPHPA WAKABIDHIWA MAABARA YA KISASA ILIYOGHARIMU BIL.3.8, KATIBU MKUU WIZARA YA KILIMO ATOA MAAGIZO

Kanda ya Kaskazini yatolewa kimasomaso na TPHPA Mashindano ya SHIMMUTA 2024//Yatwaa Mataji Matatu huku ikiweka rekodi Maalumu