TPHPA yaichapa bila huruma TRA mchezo wa Darts wanawake, yatinga fainali Michezo miwili











TPHPA Tanga

Novemba 17, 2024 – Mkoani Tanga Mfanyakazi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Bi. Rehema Abdala, leo ameonyesha ufanisi mkubwa katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi, na Makampuni Binafsi yanayoendelea mkoani hapa, kwa kufanikiwa kutinga fainali ya Mchezo wa Vishale (Darts) kwa Wanawake.


Bi. Rehema Abdala alionyesha umahiri wake kwa kumshinda mchezaji kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika hatua ya Robo Fainali. Ushindi huu ulimuwezesha kutinga Nusu Fainali ambapo alikutana na mchezaji kutoka Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMT). Katika mchezo huo, Bi. Abdala alionesha umahiri mkubwa na alifanikiwa kumshinda mpinzani wake, hivyo kumfanya kuwa mchezaji wa kwanza kutinga fainali ya mchezo huo.


Fainali ya Mchezo wa Vishale (Darts) kwa Wanawake itafanyika kesho mchana, ambapo TPHPA itachuana na timu ya Shirika la Mzinga, katika siku ya ufunguzi wa mashindano haya. Mashindano ya mwaka huu ni makubwa zaidi, ambapo jumla ya Taasisi na Mashirika 91 yameshiriki, na wachezaji 40 wa kike wanashindana kwa ubora katika mchezo wa Vishale (Darts). Ushiriki huu mkubwa unaonesha jinsi michezo inavyovutia na kuchochea ushirikiano kati ya mashirika na taasisi mbalimbali nchini.


Katika hatua nyingine, mfanyakazi mwenzake kutoka TPHPA, Bi. Veneranda Edward, pia ameonyesha mafanikio makubwa. Leo hii, Bi. Veneranda alifanikiwa kutinga fainali ya Mchezo wa Bao kwa Wanawake, baada ya ushindani mkubwa katika michuano iliyofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Fainali ya Bao kwa Wanawake inatarajiwa kuchezwa kesho, majira ya saa nne asubuhi.


Mashindano haya yanayoendelea mkoani Tanga yamekuwa na ushindani mkali, huku mashirika, taasisi, na makampuni binafsi yakishiriki kwa wingi. Wachezaji kutoka maeneo mbalimbali wameonyesha jitihada kubwa, na ni dhahiri kuwa michezo hii ni jukwaa muhimu la kukuza afya, ushirikiano, na mshikamano kati ya taasisi mbalimbali.


Tunawatakia kila la heri Bi. Rehema Abdala na Bi. Veneranda Edward katika michezo yao ya fainali kesho, na tunatarajia kuona mafanikio zaidi kutoka kwa wachezaji wa TPHPA katika mashindano haya.

Comments

Popular posts from this blog

Ni TPHPA tena! yatwaa tuzo Mshindi wa Kwanza

Kanda ya Kaskazini yatolewa kimasomaso na TPHPA Mashindano ya SHIMMUTA 2024//Yatwaa Mataji Matatu huku ikiweka rekodi Maalumu

Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Apokea Makombe 6 yaliyopatikana Katika Mashindano ya Mei Mosi na SHIMMUTA 2024