Tanzania yaanza kupiga hatua mpango wa Usimamizi wa Vifungashio vya Viuatilifu//Wadau wakutana kujadili mikakati















Arusha, Disemba 12, 2024
– Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Ndunguru, amefungua kikao cha wadau kilichofanyika katika ukumbi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu jijini Arusha. Kikao hiki kililenga kutafuta suluhu bora ya usimamizi wa vifungashio vya viuatilifu, ili kuhakikisha afya ya binadamu na uhifadhi wa mazingira kwa sasa na katika siku zijazo.


Katika hotuba yake, Prof. Ndunguru alisema kwamba kutokuwepo kwa usimamizi mzuri wa vifungashio vya viuatilifu kuna hatarisha mazingira na afya ya binadamu, hasa kwa wakulima wanapotumia viuatilifu bila ya kufuata taratibu bora za usimamizi wa vifungashio hivyo.


Bwana Raphael Mwezi, Afisa Mwandamizi kutoka TPHPA, alifafanua kwamba kikao hicho kimejumuisha wadau kutoka sekta mbalimbali, akiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, wakulima, wataalamu kutoka TPHPA, na wadau wa viuatilifu. Lengo kuu la kikao hiki ni kuhakikisha njia sahihi na salama za usimamizi wa vifungashio vya viuatilifu zinazochukuliwa kwa ajili ya kulinda afya ya wakulima na mazingira.


Bwana Mwezi aliongeza kuwa hatua ya Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu ni muhimu kwa kuwa inahakikisha kwamba vifungashio vya viuatilifu vinakusanywa hivyo kuepuka madhara yanayotokana na uharibifu wa mazingira na athari za kiafya, alieleza kuwa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu kwa kushirikiana na wadau, imefanikiwa kujenga vibada 12 katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, kama sehemu ya juhudi za kukusanya vifungashio vya viuatilifu vilivyotumika.


 Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa vifungashio hivyo havileti madhara kwa mazingira na afya ya binadamu.


Katika kikao hicho, wadau walipata fursa ya kujadiliana na kutoa mapendekezo ya jinsi ya kuboresha usimamizi wa vifungashio vya viuatilifu, ikiwa ni pamoja na njia za kuboresha uhamasishaji kwa wakulima na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kutunza vifungashio hivyo kwa usalama.


Kikao hicho kilikuwa na umuhimu mkubwa kwa sekta ya kilimo, afya na mazingira nchini, na kinatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika usimamizi wa viuatilifu na kuhakikisha usalama wa wakulima na mazingira kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

Ni TPHPA tena! yatwaa tuzo Mshindi wa Kwanza

TPHPA WAKABIDHIWA MAABARA YA KISASA ILIYOGHARIMU BIL.3.8, KATIBU MKUU WIZARA YA KILIMO ATOA MAAGIZO

Kanda ya Kaskazini yatolewa kimasomaso na TPHPA Mashindano ya SHIMMUTA 2024//Yatwaa Mataji Matatu huku ikiweka rekodi Maalumu