Wakulima wa Mbogamboga, Matunda na Maua Wapata Mafunzo ya Matumizi Sahihi ya Viuatilifu
![]() |
Arusha, Tanzania 1 Disemba 2024 Wakulima wa mbogamboga, matunda, maua na viungo kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania wamepatiwa mafunzo ya kina kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu katika kilimo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha uzalishaji na uhifadhi wa mazingira. Mafunzo hayo yalifanyika kwa siku mbili katika Kituo cha TAHA kilichopo Viwanja vya Nanenane, Mkoani Arusha, na yalihusisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya kilimo.
Mafunzo hayo yalifadhiliwa na Serikali ya Uholanzi kwa kushirikiana na TPHPA (Tanzania Plant Health and Pesticides Authority) pamoja na TAHA (Tanzania Horticultural Association). Lengo kuu lilikuwa kuwajengea wakulima uwezo wa kutambua na kudhibiti visumbufu mashambani, hasa wadudu na magonjwa, kwa njia salama na endelevu, huku wakizingatia usalama wa mazingira na afya za walaji.
Wakulima walifundishwa jinsi ya kutambua visumbufu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wadudu, magonjwa, na kuvu vinavyoathiri mazao yao ya mbogamboga, matunda, maua, na viungo. Pia walijifunza kuhusu mbinu bora za kutumia viuatilifu na wakati muafaka wa kufanya unyunyiziaji ili kudhibiti visumbufu hivyo.
“Katika kilimo cha kisasa, ni muhimu kutumia viuatilifu kwa usahihi na kwa wakati unaofaa. Hatupaswi kutumia kemikali nyingi zaidi ya zinazohitajika, kwani hii inaweza kuwa hatari kwa afya zetu na mazingira,” alisema Ndug. James Simon, mtaalamu kutoka TPHPA, aliyeongoza mafunzo hayo.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa TPHPA wa kukuza kilimo endelevu na salama hapa nchini, Mamlaka imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia wakulima, hasa katika masuala ya kilimo cha mbogamboga na matunda.
Washiriki walifurahia mafunzo haya na walionyesha hamu kubwa ya kutumia mbinu mpya zilizofundishwa. Wakulima wengi walikiri kuwa elimu ya matumizi sahihi ya viuatilifu ni muhimu kwa kuongeza uzalishaji wa mazao bora na salama, huku wakiepuka athari zinazoweza kutokea kutokana na matumizi mabaya ya kemikali.
“Nilikuwa siijui vizuri aina ya viuatilifu na ni lini niwe nayatumia. Sasa nimeshafahamu jinsi ya kufanya unyunyiziaji na ni wakati gani sahihi wa kufanya hivyo ili kuepuka madhara kwa mazao na mazingira
Comments
Post a Comment