TPHPA YASISITIZA UTUNZAJI WA MBEGU ZA ASILI
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Taifa Cha Hifadhi ya Nasaba za Mimea (NPGRC) Dkt. Sospeter Mujuni Kabululu wakati alipotembelewa na ugeni wa wataalamu kutoka Lusaka Zambia ambao wametembelea TPHPA kwa ajili ya kujifunza masuala ya namna ya utunzaji na uzalishaji wa mbegu za asili ambapo Kaimu huyo amebainisha kuwa mbegu za asili ni muhimu kutunza kwa ajili ya matumizi ya baadae kwani itasaidia kama akiba ambapo kwa sasa mbegu hizi zimekuwa zikipotea kadri muda unavyozidi kwenda.
Akifafanua zaidi Dkt. Kabululu amesema imekuwa ni kawaida kwa jamii ya sasa kutumia mbegu za kununua madukani ambapo kabla hazijaoteshwa zinapitia utafiti wa kimaabara kwa ajili ya chunguzi mbalimbali kuhusu ufanisi wake katika uzalishaji haswa wa mazao ya chakula na biashara, na kuacha matumizi mbegu za asili kwa mtazamo wa kwamba hazina ufanisi ukilinganisha na mbegu hizo za kisasa.
Ameongeza kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nasaba za Mimea haijabaki nyuma kwa kuendelea kutafuta, kuhifadhi na kuzalisha mbegu hizi za asili kwa faida ya wakulima na jamii kiujumla,
Pia ametoa wito kwa jamii kuwa wanatakiwa kutumia mbegu za asili kwani zinamatokeo mazuri kwa mazao ya chakula na lishe bora.
Akitaja sababu za kuvutiwa kuja kutembelea Kituo hiki hapa Tanzania amesema ugeni ulihamasishwa na namna ambavyo Wawakilishi kutoka Tanzania walivyowasilisha utendaji wa kazi na mipango ya utekelezaji katika Mikutano mikubwa inayojumuisha nchi zote 16 za ukanda wa Kusini mwa Africa namna kazi zinavyofanyika hapa nchini hivyo wakavutiwa na kuamua kufika kujionea wenyewe.
Aidha mmoja wa wageni ambae ni Mkuu wa Hifadhi ya Nasaba za Mimea (SPGRC) kutoka Lusaka Zambia Bi. Tilabilenji Phiri Akiongea wakati wa ziara hiyo amesema
uhifadhi wa Mbegu hizi za Asili utawezesha wakulima na watafiti kupata sifa mbalimbali za mazao na hivyo kuhakikisha usalama wa chakula na lishe bora siku za mbeleni"
Nae Bi. Peggi Ng'ono Msimamizi wa Uhifadhi kutoka SPGRC ambae pia ni mmoja wa wageni hao aliongeza kuwa wameridhishwa na uendeshaji wa shughuli zote zinazofanyika katika kuendeleza na kuhamasisha wakulima kutumia Mbegu za Asili kwani tafiti zinaonesha kwamba zaidi ya asilimia 90 ya uzalishaji wa chakula na upatikanaji wa lishe bora unachangiwa na Mbegu za Asili.
Katika Kipindi chote cha ziara, wataalamu hawa walipata nafasi ya kujionea namna NPGRC inavyoendeleza uzalishaji wa mbegu hizi za Asili karibu na maeneo ambayo kuna shughuli kubwa za kilimo kwa kuanzisha Benki za Jamii ambazo zinarahisisha upatikanaji wa mbegu hizo kwa wakulima wa ngazi zote.
Wataalamu hawa kutoka Lusaka Zambia walhitimisha ziara yao ya Siku tano kwenye Makao Makuu ya Mamlaka yaliyopo Ngaramtoni mkoani Arusha 31 Januari 2025 kwa kutembelea vituo mbalimbali vinavyoendeleza uzalishaji wa Mbegu za Asili na Mazao ya Chakula vikiwemo vituo vilivyopo katika Kijiji cha Slahhamo na Kijiji cha Kambi ya Simba Wilayani Karatu mkoani Manyara.
Comments
Post a Comment