TPHPA YAFANYA UKAGUZI KATIKA MASHAMBA MAKUBWA KANDA YA KASKAZINI, WAKULIMA WAFURAHIA UKAGUZI






Wataalam kutoka Tanzania Plant Health and Pesticides Authority (TPHPA)wapo Kanda ya Kaskazini katika Ziara ya ukaguzi kwenye mashamba makubwa mbalimbali ya mazao yasafirishwayo nje ya nchi  ikiwa ni sehemu ya juhudi endelevu za kuhakikisha uzalishaji wa mazao unafuata viwango vya ubora na usalama kwa soko la ndani na kimataifa.

Ziara hii inahusisha Ukaguzi wa matumizi ya viuatilifu, udhibiti wa wadudu waharibifu, mifumo ya umwagiliaji, mbinu bora za kilimo na utoaji ushauri katika changamoto wanazokutana nazo wakulima ikiwepo magonjwa yanayoikumba mimea .

Katika ziara hii, wataalam wanatembelea mashamba makubwa ya wakulima takriban 25 wanaosafirisha bidhaa zao nje ya nchi ambapo wanashuhudia maendeleo makubwa yaliyotokana na ushauri wa kitaalam unaotolewa na TPHPA.

Akizungumza kuhusu  Ukaguzi huu Mtaalam wa TPHPA ndugu Jumanne Mgana amesema malengo ya ukaguzi  katika mashamba hayo ni kukagua mimea na uwepo wa visumbufu vya Karantini na magonjwa yanayoweza kusababisha athari kwenye mazao yanayopelekwa nje ya nchi na kupelekea kutokukidhi vigezo , pia wataalam kujiridhisha hali ya mashamba ili wakati wa utoaji wa vyeti vya usafi wa mazao tayari  wanakuwa wana taarifa ya mashamba hayo, kupunguza na Kuondoa kabisa  ukiukwaji wa sheria (notification of noncompliance) aidha kuwasisitiza wakulima hao umuhimu wa kufuata kanuni za matumizi salama ya viuatilifu ili kulinda afya ya walaji na mazingira.  

Pamoja na hayo ndugu Jumanne amesema baada ya ukaguzi hutoa ripoti maalum ya ukaguzi ambayo wakulima hao hupaswa pia kuionyesha pindi waombapo cheti cha usafi wa mazao. 

Kwa upande wao, wakulima wa Mashamba haya makubwa wanaeleza mafanikio wanayoyapata kutokana na ushauri wa wataalam wa TPHPA, huku wakisema kuwa elimu wanayopewa inawasaidia kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao yao. Baadhi yao wanaeleza changamoto wanazokabiliana nazo, zikiwemo mabadiliko ya tabia ya nchi, wadudu waharibifu na jinsi TPHPA inavyojikita katika kusaidia utatuzi wa changamoto hizo na kuboresha zaidi uzalishaji wao.

Ziara hii ni moja ya hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa sekta ya kilimo nchini Tanzania inakua kwa kasi na kushindana katika soko la kimataifa. TPHPA inaahidi kuendelea kushirikiana na wakulima kwa kufanya ukaguzi kila mwezi na kutoa elimu na ushauri wa kitaalam ili kuhakikisha kuwa mauzo ya mazao nje ya nchi yanaongezeka, na sekta hiyo inachangia zaidi katika uchumi wa taifa.

Comments

Popular posts from this blog

Ni TPHPA tena! yatwaa tuzo Mshindi wa Kwanza

TPHPA WAKABIDHIWA MAABARA YA KISASA ILIYOGHARIMU BIL.3.8, KATIBU MKUU WIZARA YA KILIMO ATOA MAAGIZO

Kanda ya Kaskazini yatolewa kimasomaso na TPHPA Mashindano ya SHIMMUTA 2024//Yatwaa Mataji Matatu huku ikiweka rekodi Maalumu