TPHPA Yakamilisha Ziara ya baadhi ya Mashamba ya Wakulima wa Macadamia Nchi Nzima
Machi 3, 2025, wataalamu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) wamekamilisha ziara ya kutembelea baadhi ya mashamba ya wakulima wa zao la Macadamia nchi nzima. Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kutambua wakulima na kukusanya taarifa kuhusu visumbufu vya zao hilo, ikiwa ni hatua muhimu kwa ajili ya kuandaa taarifa maalumu kwa ajili ya kufungua masoko ya kimataifa.
Zoezi hilo lilifanyika katika kanda mbalimbali za Mamlaka ya Afya ya Mimea, ambapo Ndug. Godfrey Makenza, Afisa wa Mamlaka aliyekusanya taarifa kanda ya Kaskazini, alieleza kuwa zao la Macadamia limevutia wakulima kutokana na uwepo wa soko la uhakika. “Zao la Macadamia lina mvuto mkubwa kwa wakulima kutokana na soko la kimataifa linaloendelea kukua, na hili linaongeza matumaini ya faida kubwa kwa wakulima wetu," alisema Makenza.
Aidha, Makenza alibainisha kuwa ziara hii ni muhimu katika kukusanya taarifa za visumbufu vinavyoshambulia zao la Macadamia, ili kuchukua hatua sahihi za kudhibiti na kuhakikisha mazao hayo yanakidhi viwango vya ubora na usalama wa kimataifa. Hii ni hatua muhimu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo nchini, huku TPHPA ikifanya jitihada za kufungua masoko ya kimataifa kwa wakulima wa Macadamia.
Taarifa zinazokusanywa zitasaidia kuandaa mkakati wa kudhibiti magonjwa na wadudu wa Macadamia, kuboresha uzalishaji, na kuhimiza wakulima kufuata taratibu za kilimo bora ili kuhakikisha mazao yao yanapata soko lenye tija na manufaa makubwa.
Comments
Post a Comment