TPHPA yafanya ziara ya kuwajengea uwezo Wafanyabiashara wa Viuatilifu Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa namna ya kutumia mfumo wa E- Kilimo
Ziara hii imeanza rasmi Machi 24, 2025, Mkoani Mbeya na itahusisha mikoa yote inayojumuisha kanda hiyo. Lengo kuu la ziara hii ni kuwajengea uwezo wafanyabiashara wa viuatilifu katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ni Mbeya, Iringa, Njombe na Songwe ili waweze kujiandikisha na kutumia mfumo wa E-Kilimo kwa urahisi. Mfumo huu unarahisisha mchakato wa kuomba vibali na leseni kwa wadau wa kilimo na kutoa huduma mbalimbali zinazotolewa na TPHPA.
Katika ziara hiyo Wafanyabiashara watajengewa uelewa kuhusu faida za mfumo huu wa kisasa, ambao utaongeza ufanisi katika upatikanaji wa vibali halali na kusaidia kuzuia biashara za viuatilifu zisizo na vibali, hivyo kulinda afya ya mimea, mazingira, na kuhakikisha mazao yanakidhi viwango vya ubora kwa soko la ndani na la kimataifa.
Aidha, ni takwa la kisheria kwamba ili kufanya biashara ya viuatilifu nchini, lazima wafanyabiashara wawe na kibali halali kutoka TPHPA. Hivyo, kila mfanyabiashara atapaswa kufuata mchakato wa kisheria ili kuepuka adhabu na kuhakikisha kuwa biashara zao zinakuwa salama na halali.
Ziara hii ni sehemu ya juhudi za TPHPA kuboresha sekta ya kilimo nchini, kupunguza changamoto zinazowakumba wakulima, na kuhakikisha usalama wa chakula.
Comments
Post a Comment