TPHPA Yapokea Hati ya Kiwanja kwaajili ya Ujenzi wa Kituo cha Kimkakati Njombe







Machi 5, 2025 – Mbeya

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Ndunguru, amepokea rasmi hati ya kiwanja kilichonunuliwa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Kimkakati cha TPHPA Njombe. Hafla ya makabidhiano ilifanyika katika Hoteli ya Eden Highlands, mkoani Mbeya, ambapo hati hiyo ilikabidhiwa na Kaimu Meneja wa TPHPA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Kwa sasa, Kituo cha TPHPA Njombe kinaendesha shughuli zake katika ofisi zilizopo ndani ya jengo la Mkuu wa Mkoa wa Njombe, huku maandalizi ya ujenzi wa kituo cha kudumu yakiendelea. Kituo hiki kinafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Mimea ya mwaka 2020 na kanuni zake za 2023, kikiwa na jukumu la kusimamia afya ya mimea, viuatilifu, udhibiti wa visumbufu, na kuhakikisha mazao ya Tanzania yanafikia viwango vya kimataifa kwa ajili ya masoko ya nje.

Miongoni mwa shughuli zake kuu ni pamoja na ukaguzi wa maduka na maghala ya viuatilifu, mafunzo kwa wakulima, ukaguzi wa mashamba na vituo vya kufungasha mazao yanayosafirishwa nje ya nchi, pamoja na udhibiti wa magonjwa na wadudu waharibifu. Kituo pia kinahusika na utoaji wa huduma za maabara, kusimamia fumigation, na kuwaelimisha wakulima juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu.

Tangu kuanzishwa kwake, kituo kimepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa hati miliki ya kiwanja kwa ajili ya ujenzi wake, kuanzishwa kwa ofisi mpya, na kutoa mafunzo kwa wakulima zaidi ya 1,000 katika mikoa ya Njombe, Iringa, Songwe, na Mbeya. Pia, kimefanikiwa kudhibiti milipuko ya viwavijeshi na kuendelea na tafiti za kuboresha uzalishaji wa parachichi na mazao mengine.

Hatua hii ya kupatikana kwa kiwanja ni mafanikio makubwa kwa TPHPA, ikidhihirisha dhamira yake ya kuimarisha sekta ya kilimo nchini kwa kuhakikisha usimamizi bora wa afya ya mimea na mazao kwa ustawi wa wakulima na uchumi wa taifa.

Comments

Popular posts from this blog

Ni TPHPA tena! yatwaa tuzo Mshindi wa Kwanza

Kanda ya Kaskazini yatolewa kimasomaso na TPHPA Mashindano ya SHIMMUTA 2024//Yatwaa Mataji Matatu huku ikiweka rekodi Maalumu

Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Apokea Makombe 6 yaliyopatikana Katika Mashindano ya Mei Mosi na SHIMMUTA 2024