TPHPA yawakutanisha wadau Dodoma kuthibitisha Mkakati wa Taifa wa Udhibiti wa Ugonjwa wa Fungashada ya Migomba








Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kwa ushirikiano na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO), kupitia mradi wa STREHIT,Machi 13, 2025 imewakutanisha wadau mbalimbali katika Ukumbi wa Mikutano wa Mesuma Hoteli, Dodoma, ili kupitia, kujadili, kutoa mapendekezo, na kuthibitisha Mkakati wa Taifa wa Udhibiti wa Ugonjwa wa Fungashada ya Migomba (BBTV). Mkutano huu ulifunguliwa na Ndugu Musa Chidinda,Kaimu Meneja wa Usimamizi wa Usafi wa Mimea na Karantini ya Taifa(TPHPA) akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph Ndunguru.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano, Ndugu Musa Chidinda alisema, "Ugonjwa wa Fungashada ya Migomba ni tishio kwa uzalishaji wa ndizi nchini, zao ambalo ni muhimu kwa lishe, kipato cha wakulima, na uchumi wa taifa kwa ujumla. Serikali kupitia TPHPA imechukua hatua madhubuti kuhakikisha tunapambana na ugonjwa huu kwa njia mbalimbali, ikiwemo utoaji wa elimu kwa wakulima, uangamizaji wa migomba iliyoathirika, na usambazaji wa miche salama."

Hata hivyo, Chidinda alisisitiza kwamba ugonjwa huu bado haujadhibitiwa kikamilifu, na kwamba mkutano huu ni muhimu kwa ajili ya kuthibitisha mkakati wa kitaifa wa kudhibiti ugonjwa huu ili kulinda kilimo cha migomba kwa vizazi vijavyo.

Tangu mwaka 2021, ugonjwa wa Fungashada ya Migomba ulibainika kwa mara ya kwanza Wilayani Buhigwe, Mkoa wa Kigoma. Ugonjwa huu unasababishwa na virusi vya jamii ya Babuvirus kutoka familia ya Nanoviridae na huenea kupitia machipukizi yaliyoathirika pamoja na wadudu mafuta (Pentalonia nigronervosa)

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania inaendelea na jitihada mbalimbali kukabiliana na ugonjwa huu na imeandaa Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Fungashada ya Migomba, ambao kwa sasa upo katika hatua za kuthibitishwa.

Comments

Popular posts from this blog

Ni TPHPA tena! yatwaa tuzo Mshindi wa Kwanza

TPHPA WAKABIDHIWA MAABARA YA KISASA ILIYOGHARIMU BIL.3.8, KATIBU MKUU WIZARA YA KILIMO ATOA MAAGIZO

Kanda ya Kaskazini yatolewa kimasomaso na TPHPA Mashindano ya SHIMMUTA 2024//Yatwaa Mataji Matatu huku ikiweka rekodi Maalumu