TPHPA YATUMIA KONGAMANO LA PEMBEJEO MKOANI MBEYA KUWAASA WAKULIMA JUU YA MATUMIZI SAHIHI NA SALAMA YA VIUATILIFU
Akifungua Kongamano hilo litakalofanyika kwa siku mbili Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Zuberi amewapongeza taasisi ya CropLife Tanzania kwa kuandaa kongamano hilo mkoani hapo kwani litawasaidia wakulima wengi kwa kuwaongezea uwezo na kuzidi kuimarisha uzalishaji wa mazao bora ya biashara pamoja na chakula.
Ikiwa kama mshiriki mkuu wa Kongamano hilo, Mamlaka ya Afya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imetumia uwanja wa Kongamano hilo kuwafundisha wakulima matumizi Sahihi na Salama ya Viautilifu, Utambuzi wa visumbufu mbalimbali pamoja na njia za kuwadhibiti.
Mdhibiti Ubora wa Viuatilifu kutoka TPHPA Ndg.Ramadhani Kilewa amewaasa wakulima kuzingatia maelezo yanayoandikwa kwenye vibandiko vya viuatilifu ili kuepusha matumizi ya Viuatilifu bandia, Kukosea na kutumia kiuatilifu kisichoendana na zao au visumbufu husika na pia Kujikinga dhidi ya Madhara yatokanayo na kutotumia viuatilifu kwa Usahihi na Usalama kwani viuatilifu hivi ni Sumu.
Uwepo wa TPHPA Kongamano hilo unasisitiza dhamira yao ya sio tu kudhibiti viuatilifu bali pia kukuza utamaduni wa matumizi salama na uwajibikaji ndani ya jumuiya ya kilimo kwa kushirikiana moja kwa moja na wakulima na wadau wengine wa kilimo ambapo TPHPA inalenga kuongeza uelewa, kujenga uwezo, na hatimaye kuchangia katika kanuni za kilimo bora na uzalishaji salama wa chakula nchini Tanzania.
Kongamano hili lenye Kauli mbiu ya “Kuelekea Dira ya 2050 – Pembejeo Sahihi kwa Chakula Salama” limeanza leo tarehe 25 Aprili 2025 na kufikia tamati hapo kesho na pia limeambatana na maonesho madogo kwa Taasisi Zilizoshiriki kongamano hilo kupata nafasi ya kuonesha Huduma na Bidhaa wanazozizalisha kwa faida ya Mkulima.
Comments
Post a Comment