TPHPA YADHIBITI HATARI YA UHARIBIFU WA MPUNGA MASHAMBANI :
Yatoa Elimu utegaji Sumu ya Panya mashambani na kusimamia Uchanganyaji wa sumu na Chambo Zanzibar
Katika kuhakikisha usalama wa binadamu, mifugo, na mazingira wakati wa kudhibiti panya mashambani, Wataalam kutoka TPHPA wametoa elimu ya tahadhari kwa wakulima wa Zanzibar kabla ya kuweka sumu ya kuua panya kwenye mashamba yao.
Zoezi hili limefanyika katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar likiwemo eneo la Bumbwisudi, Cheju na Kilombero. Wakulima walipokea mafunzo ya kina kuhusu matumizi salama ya sumu, hatua za kuchukua ili kujikinga na madhara, na umuhimu wa kushirikiana na wataalamu katika hatua zote za utegaji.
Wataalam hao walisisitiza tahadhari muhimu kama kuhakikisha Sumu haitumiki ndani ya nyumba, kuwepo kwa alama ya kitambaa chekundu katika Shamba lililotegwa sumu ili kujulisha hatari katika eneo hilo, Watoto na mifugo wasikaribie eneo lenye sumu.
Vilevile Vifaa vilivyotumika kubebea au kuchanganya sumu (mfano mifuko) vichomwe moto baada ya matumizi.
Aidha, shughuli za uchanganyaji na usambazaji wa sumu zinasimamiwa kwa karibu na wataalamu wa TPHPA, kuhakikisha maelekezo ya usalama yanafuatwa kikamilifu kabla ya sumu kufikishwa mashambani.
Akiongea Mkuu wa Kituo cha Udhibiti wa panya cha TPHPA kilichopo Morogoro bi Christina amesema elimu kabla ya uchanganyaji katika chambo ni muhimu kwani kumekuwa na hatari nyingi likiwemo vifo kutokana na ukosefu wa elimu sahihi juu ya matumizi yasiyo sahihi ya sumu hizi.
Wakulima waliopokea elimu hiyo waliishukuru TPHPA kwa kuwapa maarifa muhimu. “Hatukuwa tunajua madhara ya kutumia sumu bila tahadhari. Sasa tumeelimika, tutaweka alama, na kuchukua hatua za kujilinda sisi na familia zetu,” alisema mmoja wa wakulima wa Bumbwisudi.
Kwa hatua hii, TPHPA inachangia moja kwa moja katika utekelezaji wa Agenda 10/30 ya Serikali inayolenga kuongeza tija katika kilimo kwa kutumia teknolojia salama na kuongeza ushiriki wa wakulima katika kilimo bora chenye tija.
Udhibiti wa visumbufu kama panya ni sehemu muhimu ya kuongeza uzalishaji wa mazao na hivyo kukuza kipato cha wakulima na ni msingi wa kumfikia lengo la kiuchumi kupitia kilimo ifikapo mwaka 2030.
Comments
Post a Comment