TPHPA yaanza mpango wa kibaiolojia Kunusuru Ziwa Victoria Dhidi ya Gugu Maji
Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kupitia maabara zake za kisasa zilizopo katika Kituo cha Udhibiti wa Visumbufu vya Mimea Kibiolojia, Kibaha, mkoani Pwani, imeanza kuzalisha mdudu rafiki wa mazingira aina ya "mbawa kavu" (Cyrtobagous salviniae) kwa ajili ya kudhibiti gugu maji vamizi (Salvinia molesta). Gugu hilo limekuwa tatizo kubwa katika Ziwa Victoria na vyanzo vingine vya maji hapa nchini, likisababisha athari kwa usafiri, mazingira, uchumi na maisha ya jamii zinazotegemea ziwa hilo.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa zoezi hilo, tarehe 18 Julai 2025, Mkurugenzu wa Usalama wa Afya ya Mimea TPHPA, Dkt. Benignus Ngowi, amesema matumizi ya mdudu rafiki huyo ni sehemu ya mkakati endelevu wa kutumia mbinu za kibaiolojia kudhibiti visumbufu bila kuathiri mazingira. Alibainisha kuwa njia hiyo ni salama, rafiki kwa viumbe hai wengine na inaweza kusaidia kupunguza gharama kubwa zinazotumika katika kudhibiti magugu hayo.
Kwa upande wake, Ndugu Keneth Nyakunga, mtaalamu na afisa mwandamizi wa udhibiti wa visumbufu kwa njia ya kibaiolojia alisema kuwa mdudu rafiki huyo “mbawa kavu” (Cyrtobagous salviniae) waliletwa kwa ushirikiano na Serikali ya Uganda, ambako tayari wametumika kwa mafanikio makubwa nchini Uganda katika kudhibiti gugu maji vamizi (Salvinia molesta). Kwa upanda wa Tanzania kwa sasa wapo katika hatua ya kumchunguza kwa kina tabia zake ikiwa ni pamoja na usalama wake katika mazingira pamoja na ufanisi na baadae kuwazalisha kwa wingi kabla ya kuanza kuwasambaza katika maeneo yaliyoathirika zaidi na gugu hilo, ili kudhibiti tatizo hilo kwa ufanisi na kwa njia endelevu.
Comments
Post a Comment