TPHPA yazidi kuimarisha wataalamu wake Juu ya Matumizi ya Drone//Watangaza fursa kwa Wakulima
Arusha, Julai 24, 2025 — Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imepokea rasmi ripoti ya wataalamu wake waliorejea kutoka nchini Kenya walikokuwa wakipata mafunzo ya juu kuhusu matumizi ya ndege nyuki (droni) kwa ajili ya uchunguzi wa afya ya mimea kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya Advanced Photogrammetry Intelligence. Hafla ya upokeaji wa ripoti hiyo imefanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya TPHPA zilizopo jijini Arusha.
Teknolojia ya Advanced Photogrammetry Intelligence inahusisha matumizi ya picha za angani zinazopigwa na droni kwa ajili ya kuchambua kwa usahihi hali ya mimea, udongo, na miundombinu ya mashamba. Kupitia mbinu hiyo, TPHPA inalenga kuboresha mifumo ya ulinzi wa mimea nchini kwa kutumia teknolojia za kisasa zinazoendana na mabadiliko ya hali ya hewa na changamoto nyingine katika kilimo.
Kwa sasa, TPHPA inamiliki jumla ya droni 20 zilizotengwa mahsusi kwa ajili ya shughuli za uchunguzi wa afya ya mimea na usimamizi wa mashamba. Droni hizo zitatumika katika maeneo mbalimbali ya kilimo nchini, chini ya usimamizi wa wataalamu waliopatiwa mafunzo maalum, ili kutoa taarifa za kisayansi zitakazosaidia kufanya maamuzi sahihi katika uzalishaji wa mazao.
Huduma hii inalenga kuwahudumia wakulima wadogo na wakubwa, vikundi vya wakulima, taasisi za kifedha zinazotoa mikopo ya kilimo, pamoja na mashirika na taasisi za utafiti wa kilimo na afya ya mimea. Kwa kutumia droni hizo, wakulima wataweza kufuatilia maendeleo ya mazao yao, kugundua magonjwa ya mimea mapema, kuchambua afya ya mimea, kupima hali ya udongo, kudhibiti visumbufu na magonjwa, pamoja na kusimamia matumizi ya maji kwa ufanisi mkubwa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka TPHPA, matumizi ya teknolojia hii yataongeza tija ya uzalishaji mashambani, kupunguza hasara kwa wakulima, na kuimarisha uwezo wa kufanya maamuzi ya kilimo kwa kuzingatia taarifa sahihi za kisayansi. Mamlaka hiyo inatoa wito kwa wakulima na wadau wote wa sekta ya kilimo nchini kuwasiliana nao kwa ajili ya kupata huduma, mafunzo, na usaidizi kuhusu matumizi ya teknolojia hiyo mpya. Na Kwasasa Mamlaka inazo ndege nyuki (Drone) zipatazo 20 maalumu kwaajili hiyo.
Comments
Post a Comment