TPHPA Yazidi kupiga Hatua katika Matumizi ya Teknolojia za Kisasa Kudhibiti Visumbufu na Kuimarisha Biashara ya Mazao Nchini
Akizungumza tarehe 30 Julai 2025 katika Makao Makuu ya TPHPA jijini Arusha, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, alisema kuwa mamlaka imenunua vifaa 20 vya Kichambuzi cha Vinasaba Kinachobebeka ambavyo vitasambazwa kwenye vituo vya mamlaka vya mipakani ili kurahisisha ukaguzi wa mazao yanayoingia na kutoka nchini. Baadhi ya vifaa hivyo pia vitatumika kutoa huduma za kitaalamu kwa taasisi na wadau mbalimbali, hatua itakayosaidia kuongeza mapato ya ndani na kupanua huduma za kisayansi katika sekta nyingine kama mazingira, udongo, afya na wanyama.
Prof. Ndunguru alieleza kuwa teknolojia hiyo ina uwezo wa kuchambua vinasaba vya virusi, fangasi, bakteria na wadudu kwa usahihi mkubwa. Hii inamwezesha mtaalamu kutoa mapendekezo ya kudhibiti kisumbufu kwa njia sahihi na inayolengwa, sambamba na kupunguza matumizi ya viuatilifu visivyofaa—hivyo kulinda mazingira na kupunguza gharama kwa wakulima.
Mbali na matumizi ya kilimo, Kichambuzi cha Vinasaba Kinachobebeka kina matumizi mapana katika sekta nyingine. Katika mazingira, hutumika kuchambua udongo, maji, na kufuatilia vimelea hatarishi kwa mazingira. Katika afya ya binadamu, hutumika kuchambua vinasaba vya virusi na bakteria wanaosababisha magonjwa, hivyo kusaidia kudhibiti milipuko na kusaidia katika kutoa tiba sahihi. Kwa upande wa afya ya wanyama, huchambua microbiome na kugundua vimelea wanaosababisha magonjwa, huku pia ikitumika kutathmini afya ya udongo kwa kuchambua viumbe muhimu kwa ukuaji wa mimea.
Katika muktadha wa biashara ya mazao na usalama wa chakula, kifaa hiki husaidia kugundua viumbe hatari kabla ya mazao kufika sokoni au kuvuka mipaka, hatua inayoongeza ubora, usalama, na ushindani wa bidhaa za kilimo za Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Kwa kuanza kutumia teknolojia hii, Tanzania inaingia rasmi kwenye ramani ya nchi zinazotumia mbinu za kisasa kuthibitisha ubora wa mazao. Prof. Ndunguru alisisitiza kuwa teknolojia hii inachochea tafiti mpya, kuimarisha usalama wa chakula, na kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo, biashara ya mazao, na hatimaye uchumi wa taifa.
Comments
Post a Comment