TPHPA Yaandika Historia: NPPO ya Kwanza Duniani Kutumia Teknolojia ya Portable DNA Sequencer Kutatua Changamoto za Kilimo











Agosti 6, 2025 — Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Ndunguru, ameongoza hafla ya uzinduzi wa matumizi ya teknolojia mpya ya Portable DNA Sequencer katika banda la TPHPA, kwenye Maonesho ya Nanenane yanayoendelea Viwanja vya Nzuguni, Dodoma.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Prof. Ndunguru amesema kuwa TPHPA kupitia Mradi wa Kuimarisha Huduma za Afya ya Mimea na Usalama wa Chakula (STREPHIT) imenunua vifaa 20 vya Portable DNA Sequencer. Vifaa hivyo vitatumika katika maabara na moja kwa moja mashambani kwa ajili ya uchunguzi wa haraka wa vinasaba vya viumbe mbalimbali. Amefafanua kuwa teknolojia hiyo haitumiki tu kubaini visumbufu vya mimea, bali pia husaidia katika tafiti za udhibiti wa magonjwa ya mimea, ufuatiliaji wa usalama wa chakula, na usimamizi wa ubora wa mazao kabla ya kuingia sokoni au kusafirishwa.


Prof. Ndunguru amesisitiza kuwa matumizi ya kifaa hiki ni mapinduzi makubwa kwa sekta ya kilimo, kwani yatawawezesha wataalamu kufanya uchunguzi wa kitaalamu kwa wakati sahihi, moja kwa moja mashambani. Hili litawasaidia wakulima kupata suluhisho la haraka na sahihi dhidi ya changamoto za visumbufu, magonjwa ya mimea, na matatizo ya ubora wa mazao. Ameongeza kuwa TPHPA inalenga kuwa Best NPPO (National Plant Protection Organization) in Africa ndani ya miaka mitatu ijayo, kupitia matumizi ya sayansi na teknolojia katika kulinda afya ya mimea na chakula.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usalama wa Afya ya Mimea, Dkt. Benignus Ngowi, amesema kuwa teknolojia hii imekuja kwa wakati mwafaka kwani kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakikabiliwa na magonjwa na visumbufu vya mimea vilivyokuwa vigumu kubainika mapema. "Kupitia kifaa hiki, sasa tuna uwezo wa kutambua chanzo cha tatizo kwa haraka zaidi, jambo ambalo litatusaidia kuchukua hatua mapema na kwa usahihi. Suluhisho limepatikana, na wakulima watanufaika moja kwa moja," amesema Dkt. Ngowi.

Comments

Popular posts from this blog

Ni TPHPA tena! yatwaa tuzo Mshindi wa Kwanza

Kanda ya Kaskazini yatolewa kimasomaso na TPHPA Mashindano ya SHIMMUTA 2024//Yatwaa Mataji Matatu huku ikiweka rekodi Maalumu

Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Apokea Makombe 6 yaliyopatikana Katika Mashindano ya Mei Mosi na SHIMMUTA 2024