TPHPA Yaelimisha darasa la Wakulima walioratibiwa na SAGCOT Juu ya Mbinu Bora za Upigaji Sumu kwenye Mimea viwanja vya Nane Nane – Morogoro

 USHIRIKIANO TPHPA NA SAGCOT WAIMARIKA ZAIDI,WAFANYA USHIRIKIANO KUFUNDISHA WAKULIMA 



Wakulima kutoka maeneo mbalimbali ya Morogoro wamepata fursa ya kunufaika na mafunzo muhimu yaliyotolewa na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) katika banda darasa la SAGCOT lililopo katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea  Viwanja vya Mwl.Julius Nyerere Morogoro.

Kupitia Mtaalamu wake aliebobea Ndg. Samweli Mmari Mkaguzi wa Viuatilifu, TPHPA imetoa elimu ya kina juu ya mbinu bora za upigaji wa viuatilifu katika mimea, ikiwa ni sehemu ya juhudi za mamlaka hiyo kuhakikisha wakulima wanatumia viuatilifu kwa usahihi, salama na kwa tija katika kukabiliana na visumbufu vya mazao.

Katika mafunzo hayo, wakulima walifundishwa namna bora ya:Kutambua aina sahihi ya viuatilifu kulingana na aina ya visumbufu,Kupima na kuchanganya viuatilifu kwa uwiano unaofaa,Kutumia vifaa vya kisasa vya kupulizia viuatilifu kwa ufanisi zaidi,Kujikinga kiafya wakati wa kupulizia (Personal Protective Equipment - PPE) na Kutunza mazingira kwa kuepuka matumizi holela ya sumu.

Wakulima pia walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata majibu ya kitaalamu moja kwa moja kutoka kwa Afisa wa TPHPA, huku wakionesha hamasa kubwa ya kujifunza na kuahidi kubadilisha mbinu wanazotumia mashambani.

 “Mafunzo haya yamenisaidia sana kuelewa kwanini nilikuwa sipati matokeo mazuri licha ya kutumia viuatilifu,” alisema mmojawapo wa wakulima waliotembelea banda hilo. “Sasa najua namna ya kutumia kwa usahihi na salama.”

Pamoja na hayo wameiomba Mamlaka kuendelea kujikita katika kutoa mafunzo kwa wakulima hasa vijijini kwani wamekuwa wakaihudumia wakitumia viuatlifu  kwa njia zisizofaa zinazopelekea kutopata matokeo mazuri.

Akitoa mafunzo hayo Mr Mmari amesema elimu hiyo inalenga kusaidia wakulima kuongeza uzalishaji kwa kutumia mbinu sahihi za udhibiti wa visumbufu, bila kuathiri afya ya binadamu wala mazingira.

“Lengo letu ni kuhakikisha viuatilifu vinatumika kwa njia inayoongeza tija ya mazao na kulinda afya ya mtumiaji na mazingira. Tunawasisitiza wakulima wafuate maelekezo ya wataalamu na watumie viuatilifu vilivyosajiliwa pekee,” alisema Mr.Mmari kutoka TPHPA.


TPHPA imekuwa ikitumia jukwaa la maonesho ya Nane Nane kama sehemu ya kufikia wakulima kwa wingi, kubadilishana maarifa, na kuimarisha uelewa wa masuala ya afya ya mimea nchini.

Comments

Popular posts from this blog

Ni TPHPA tena! yatwaa tuzo Mshindi wa Kwanza

Kanda ya Kaskazini yatolewa kimasomaso na TPHPA Mashindano ya SHIMMUTA 2024//Yatwaa Mataji Matatu huku ikiweka rekodi Maalumu

Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Apokea Makombe 6 yaliyopatikana Katika Mashindano ya Mei Mosi na SHIMMUTA 2024