TPHPA Yaendelea Kuwafikia Wadau wa Kilimo Nane Nane – Yatoa Elimu kwa Wakulima, Wanafunzi, Watunga Sera na Wafanyabiashara
Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA) inaendelea kushiriki kikamilifu katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yanayofanyika kitaifa kwenye Viwanja vya Nzuguni, Dodoma. Leo, tarehe 3 Agosti 2025, wataalamu wa Mamlaka wameendelea kutoa elimu na ufafanuzi kwa wadau mbalimbali wanaotembelea banda la TPHPA, wakiwemo wakulima, watunga sera, wanafunzi na wafanyabiashara.
Kupitia mawasilisho ya kitaalamu na maonyesho ya vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa visumbufu vya mimea, TPHPA inawaelimisha wadau kuhusu majukumu yake ya msingi ikiwa ni pamoja na udhibiti wa magonjwa ya mimea, ukaguzi na usajili wa viuatilifu, pamoja na hifadhi ya nasaba za mimea kupitia Kituo cha Hifadhi ya Nasaba za Mimea. Wakulima wanapata elimu juu ya matumizi salama ya viuatilifu na namna ya kutambua bidhaa gushi, huku wanafunzi wakihimizwa kushiriki katika tafiti na matumizi ya teknolojia bunifu katika kilimo.
Watunga sera wanapewa taarifa kuhusu mwelekeo wa kisera wa Mamlaka na mafanikio katika kulinda afya ya mimea na kuhakikisha usalama wa chakula nchini. Kwa upande wao, wafanyabiashara wa mazao na pembejeo wanapata maelezo kuhusu taratibu za usajili, viwango vya ubora, na fursa za kushirikiana na TPHPA katika kukuza kilimo salama na chenye tija. Ushiriki wa TPHPA katika maonesho haya unaendelea kuonesha dhamira ya dhati ya Mamlaka kushirikiana na wadau wote katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini kwa misingi ya sayansi, usalama na uendelevu.
Comments
Post a Comment